Wadau wa vyama vya akiba na Mikopo, vyama vya kilimo na masoko kutoka Zanzibar wakiongozwa na wataalamu kutoka katika Wizara ya kazi, uwezeshaji, wazee, vijana, wanawake na watoto Zanzibar wamefanya ziara ya kujifunza namna vyama hivyo vinavyofanya kazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.
Katika ziara hiyo ambayo imefadhiliwa na Programu ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF), walipata nafasi ya kutembelea vyama vya kilimo na masoko (AMCOS) na akiba na Mikopo (SACCOS) vya Ibumila pamoja na Ninga zilizopo wilayani Njombe.
Wakiwa wilayani hapa wamejifunza namna mfumo wa stakabadhi gharani unavyoendeshwa , SACCOS zilivyojikita katika utoaji wa huduma za kifedha, utoaji wa mikopo na urejeshaji wake, namna AMCOS zilivyojikita katika kukusanya mazao na kuwatafutia masoko wanachama wake pamoja na ushirikiano uliopo baina ya vyama vya akiba na mikopo pamoja na serikali za vijiji.
Akizungumzia namna Halmashauri ya wilaya ya Njombe inavyozisaidia SACCOS na AMCOS, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Monica Kwiluhya alisema kuwa Halmashauri imekuwa ikipitishia fedha za kuwezesha vikundi vya vijana na wanawake katika SACCOS jambo ambalo linaziongezea Saccos wanachama pamoja na kurahisisha ufuatiliaji upande wa Halmashauri kwa kuwa fedha hizo hufuatiliwa Saccos na sio kwa wanavikundi.
Aliongeza kuwa Mwaka huu Halmashauri imeziwezesha AMCOS kwa kuwaunganisha wanachama wake na benki ya kilimo kwa ajili ya kupata pembejeo za kilimo pamoja na kupima mashamba yote ya wanachama wa AMCOS ili kuwawezesha kupata hatimiliki za kimila zitakazowawezesha kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha kwa ajili kilimo.
“Tumepima mashamba yote ya wanachama wa AMCOS ijapokuwa ni gharama lakini kwa kuthamini umuhimu wao tumepima kwa nusu gharama ambapo fedha zinazobaki watalipa baada ya mavuno” alisema Kwiluhya.
“ Wakati wa maonyesho ya nane nane huwa tunawachukua wanachama na kuwapeleka Mbeya kwa ajili ya kuwatafutia masoko ambapo mwaka huu tumefanikiwa kuwaunganisha na wafanyabiashara kutoka katika nchi ya Botswana kwa ajili ya soko la asali” aliongeza Kwiluhya
Alifafanua kuwa AMCOS za Halmashauri ya wilaya ya Njombe zinasaidiwa kwa kutafutiwa miradi ya kuongeza thamani na kuitaja AMCOS ya Ninga kama mfano ambayo iko hatua ya mwisho kununua mashine kwa ajili ya kusaga unga na kuuza badala ya kuuza mahindi.
“Halmashauri kwa kushirikiana na mradi wa MIVARF tumejenga kiwanda kidogo cha mafunzo kwa vikundi vya wakulima kuzuia upotevu na kuongeza thamani ya mazao na kiwanda hiki kitaanza kufanya kazi mwezi Januari ” alisema Kwiluhya.
Kwa upande wake Ally Mohamed Ally ambaye ni afisa ushirika Pembe alisema kuwa wamepata uzoefu mkubwa ambao watakwenda kuutumia kuboresha utendaji kazi wa SACCOS na AMCOS Unguja na Pemba.
“Tumejifunza namna mikopo inavyotolewa, nguvu ya Halmashauri kwenye SACCOS, uhamasishaji unavyofanyika pamoja na namna SACCOS na AMCOS zinavyoshirikiana. Hakika safari yetu imekuwa ya mafanikio makubwa na tutakwenda kutekeleza kama tulivyojifunza” alisema Ally.
Nae mkuu wa wilaya ya Njombe Bi Ruth Msafiri akizungunza na ugeni huu ulipomtembelea ofisini kwake aliwataka kuyafanyia kazi yote waliyojifunza na kuacha kuchanganya siasa na masuala ya utendaji kazi.
“ Naomba mkawe waangalifu mkikosea kwenye kuchagua viongozi wazuri wa Saccos na Amcos hamtaweza kusonga mbele, mkioneana aibu na kuchangua viongozi wabovu watakuwa chanzo cha uharibifu, wizi wa mali za wanachama pamoja na kupunguza uaminifu jambo litakalochelewesha maendeleo” alisema Msafiri.
Halmashauri ya wilaya ya Njombe inajumla ya vyama vya ushirika 34, vyama vya akiba na mikopo 12 vyama vya kilimo na masoko 18. Vyama vya wafugaji vitatu, na chama cha Muungano kimoja. Hadi sasa Vyama hivyo vinamtaji wa Bilioni 3.34 huku mikopo yenye thamani ya bilioni 17.9 ikiwa imeshatolewa.
Vyama vya ushirika wilani Njombe vinajumla ya wananchama 8,384 ambapo wanaume ni 4,471 na wanawake 3153 huku kukiwa na vikundi 638 na taasisi 122.
Katika siku za hivi karibuni Halmashauri ya wilaya ya Njombe imekuwa ikitembelewa na Halmashauri mbalimbali nchini ambazo zimekuwa zikijifunza masuala mbalimbali ikiwemo kampeni ya afya na usafi wa mazingira ambapo Halmashauri ilishika nafasi ya kwanza upande wa vijiji Tanzania bara.
Tayari Halmashauri za mkoa wa Geita, Dodoma pamoja na Manispaa ya Singida zimefanya ziara ya mafunzo katika Halmashauri ya wilaya ya Njombe.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa