Katika kuboresha sekta ya elimu wilayani Njombe Halmashauri ya wilaya Njombe kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefanikiwa kuanzisha masomo ya kidato cha tano katika shule mbili za sekondari wilayani hapa.
Shule zilizopewa usajili na tayari zimeshaanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano mwaka huu ni pamoja na shule ya Sekondari Itipingi iliyopo katika Kata ya Igongolo Tarafa ya Makambako na shule ya Sekodari Lupembe iliyopo katika Kata ya Lupembe Tarafa ya Lupembe.
Shule zote mbili tayari zimepewa wanafunzi wa mchepuo wa sayansi huku Shule ya Sekondari Ipitingi ambayo imepata namba ya usajili S.1094 ikiwa na wanafunzi mchanganyiko 40 na ile ya Lupembe yenye namba ya usajili S. 0210 ikipewa wanafunzi wavulana 45.
Kufuatia kuanzishwa kwa masomo ya kidato cha tano katika shule hizo kunafanya Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kuwa na shule tatu (3) za Serikali ambazo zinazotoa masomo ya kidato cha tano ambazo ni shule ya Sekondari ya wasichana Manyunyu iliyopo katika Kata ya Matembwe, Itipingi iliyopo kata ya Igongolo na Lupembe iliyopo kata ya Lupembe huku upande wa shule za watu binafsi ni ile ya Mtwango iliyopo katika kata ya Mtwango.
Katika kuhakikisha wanafunzi wote wa shule za Sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe wanaishi katika mabweni Halmashauri imefanikiwa kuanzisha huduma ya mabweni katika Shule ya Sekondari Ninga.
Kufuatia kukamilika kwa bweni katika shule hiyo wanafunzi wa kidato cha pili na kidato cha nne wameanza kuishi katika mabweni pamoja na walimu watatu wakiamia katika nyumba za walimu zilizojengwa shuleni hapo ili kuwa jirani na wanafunzi.
Sambamba na hilo Halmashauri inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa bweni katika shule ya Sekondari Sovi kwa kushirikiana na wananchi ambapo hadi sasa zoezi la kufyatua tofali linaendelea.
Aidha , Halmashauri imeweka mipango kabambe ili kuhakikisha kila shule ya sekondari inakuwa na mabweni kwa wanafunzi wa jinsia zote ili kuinua kiwango cha ufaulu na kutokomea masuala ya mimba kwa wanafunzi wa shule za Sekondari.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa