Katikati ya mkutano mkuu wa Kijiji , wataalamu kutoka Halmashauri ya wilaya ya Njombe wanasimama na kuanza kutoa vifurushi walivyokuwa navyo.
Kila mmoja kwenye mkutano anaangalia kwa makini ni kitu gani hasa kinatolewa na hakuna ambaye anabaini mapema.
Mara kutoka kwenye moja ya vile vifurushi kinatolewa kinyesi cha binadamu mbele ya kadamnasi.
Ndio! kinyesi cha binadamu tena ambacho hakijakauka. Wananchi wanapigwa na butwaa ,wanaanza kuona kinyaa na kulalamika. Kisha mtaalam kutoka Halmashauri anawaambia wananchi kwanini wanaona kinyaa wakati kila siku wanakula kinyeshi ndio maana magonjwa ya kuhara na tumbo hayaishi miongoni mwao.
Anawaeleza kinaga ubaga kuwa kinyeshi hicho wamekitoa mita chache tu kutoka katika maeneo wanayokaa na kimetapakaa karibu kila kona.
Ni kweli kulingana na mazingira ya Njombe na mwamko mkubwa wa wananchi katika upandaji wa miti , sehemu kubwa ni misitu au mazao hivyo ni lahisi kwa wananchi kujisaidia ovyo.
Mbinu hii inaitwa Uchefuaji yaani mbinu shirikishi jamii (CLTS).
Mbinu hii ilitumika kuihamasisha jamii kuanzia ngazi ya vitongoji. Ni mbinu inayotia kinyaaa lakini yenye kuleta mafanikio.
Ili kuweza kufanikisha kampeni ya afya na usafi wa mazingira katika Halmashaur ya wilaya ya Njombe jambo la kwanza walilofanya wataalam kutoka Halmashauri ilikuwa ni kutoa elimu kwa viongozi wa ngazi za vitongoji. Kisha wakaambatana nao kusaka vinyesi na kwenda kuwachefua wananchi kwenye mkutano wa hadhara.
Baada ya kupata elimu kupitia mbinu shirikishi jamii ya uchefuaji wananchi walihamasika na kuacha kujisaidia ovyo na kujenga vyoo bora, miundombinu ya kunawia mikono kwa maji tiririka pamoja na kuvitumia vyoo hivyo.
Mbali na kuhamasika ziliundwa kamati za usimamizi wa utekelezaji kampeni ya afya na usafi wa mazingira ngazi ya Kitongoji, kijiji na Kata. Kazi kubwa ya kamati hizi ilikuwa kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara.
Sambamba na hilo timu ya ufuatiliaji kutoka Halmashauri ya wilaya ya Njombe haikuwa nyuma katika kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara na kufanya vikao na kamati za vitongoji, vijiji na Kata ili kushirikiana kutatua changamoto wazazokutana nazo katika utekelezaji wa Kampeni.
Sasa vijiji vya Sovi na Image vina kaya zenye vyoo bora kwa asilimia 100 na miundombinu ya kunawia mikono. Ndio ni kijijini lakini kuna vyoo vya sinki kama mjini.
Mazingira ya vijiji hivi kwa sasa ni safi na hakuna vinyesi vilivyotapakaa mitaani, mashambani pamoja na kwenye vichaka.
Ama kwa hakika uchefuaji kiboko!.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa