Halmashauri ya Wilaya ya Njombe imezindua chanjo kwa ajili ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi ambapo zaidi ya wasichana 1,062 wanatarajiwa kupewa chanjo wilayani hapa.
Chanjo hiyo ambayo inatolewa bure kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 itatolewa katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vilivyopo katika maeneo mbalimbali ya Kata na vijiji vya Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.
Akisoma taarifa kuhusu chanjo wakati wa uzinduzi ulifanyika katika kijiji cha Nyombo Kata ya Ikuna wilayani Njombe, Mkurugenzi mtendaji wa Halamshauri ya wilaya ya Njombe, Monica Kwiluhya alisema kuwa , wamejipanga kikamilifu katika zoezi hilo kwa kufikia zaidi ya asilimia 95 ya walengwa.
Bi kwiluhya alibainisha kwamba tayari chanjo imesambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na kuandaa orodha ya walengwa wote wanaotarajia kupata chanjo hiyo kwa mwaka 2018 ambapo wengi wao wapo katika shule za Msingi na Sekondari.
“Tumeshaandaa vituo vitakavyotoa huduma hizi kwa njia ya mkoba (outreach services) katika vijiji vyote vya Halmashauri pamoja na kutoa mafunzo ya utoaji wa chanjo kwa walimu wa shule za msingi na sekondari kutoka shule zote zilizopo katika Halmashauri” alisema Bi Kwiluhya.
Alieleza kuwa elimu na maelekezo juu ya chanjo ya kuziua saratani ya mlango wa kizazi imetolewa kwa wakuu wa idara na vitengo vya Halmashauri pamoja na kufanya uhamasishaji kwa jamii ili wananchi waweze kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo kupitia vyombo mbalimbali vya habari vinavyopatikana katika Halmashauri ya wilaya ya Njombe.
Chanjo hii itasaidia kikamilifu jitihada za kupambana na ugonjwa wa saratani ambao umekuwa ni chanzo kikubwa cha vifo vya akinamama wengi nchini. Tafiti zinaonesha kuwa saratani ya mlango wa kizazi pamoja na saratani ya matiti huchangia zaidi ya asilimia 50% ya vifo vyote vinavyosababishwa na saratani nchini.
Chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi itatolewa kwa dozi mbili kwa kila mlengwa wa chanjo ambapo mara ya kwanza itatolewa msichana anapofikisha miaka 14 na dozi ya pili itatolewa baada ya miezi 6 tangu kutolewa kwa dozi ya kwanza.
Aidha, imebainishwa na wataalamu wa masuala ya afya kuwa lazima mtu akamilishe dozi zote mbili kwa kuwa mtu akikosa dozi moja anakuwa ajakingwa
Uzinduzi wa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kitaifa ulifanywa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, jijini Daresalaam Aprili 10 mwaka 2018.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa