Halmashauri ya wilaya ya Njombe imeingia mkataba wenye thamani ya zaidi milioni 800 na mkandalasi Dynotech kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Lupembe kata ya Lupembe wilayani Njombe.
Mradi huu ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miezi nane utakuwa ni sululisho la upungufu wa maji katika Kata ya Lupembe na vitongoji vyake ambao kwa muda mrefu walikuwa wanakabiliwa nayo.
Akizungumza wakati wa utiaji wa saini mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe , Velentino Hongoli amemtaka mkandalasi kuhakikisha anafanya kazi kwa viwango na kwa wakati ili mradi uweze kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.
“ Wananchi wameusubiri mradi mkubwa kama huu kwa muda kutokana na mradi wanaoutumia kuwa mdogo na hivyo kutokidhi mahitaji yao kufuatia kijiji cha Lupembe kuwa na idadi kubwa ya watu hivyo naomba utekeleze mradi huu kwa wakati na viwango kwa muda uliopangwa” alisema Hongoli.
Aliongeza kuwa mradi ukitekelezwa kwa viwango utadumu muda mrefu na kumtaka mkandalasi kuhakikisha anazingatia na kutekelezwa kwa ubora vipengele vyote vilivyopo kwenye mkataba.
“ Leo ni mwezi wa nne naimani ifikapo januari mwaka 2020 wananachi watapata maji kwa uhakika pasipo na shaka yoyote” alisema Hongoli.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe Ally Juma ally alisema kuwa Halmashauri itausimamia kwa ukaribu mradi huu ili pesa ya serikali itumike kama ilivyokusudiwa
“ Naomba mkandalasi utekeleze mradi kwa kuzingatia viwango vya serikali na thamani ya fedha ionekane, kashirikiane vizuri na viongozi kwenye maeneo ya utekelezaji wa mradi ili mradi utekelezwa katika muda uliopangwa” alisema Ally.
Mradi huu ambao utakuwa na vituo 30 vya kuchotea maji ukikamilika utahudumia zaidi ya wakazi 6000 kutoka katika kijiji cha Lupembe na vitongoji vyake na usanifu wake utadumu kwa zaidi ya miaka 20 ijayo.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa