Halmashauri ya Wilaya ya Njombe imepokea msaada wa pikipiki 12 kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) kupitia mradi wa kukuza stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu ili kuboresha maendeleo ya elimu wilayani Njombe.
Pikipiki zilizotolewa ni aina ya Honda ambazo zimegharimu milioni 36 na zitatumiwa na waratibu elimu Kata katika kufuatilia maendeleo ya elimu kwenye shule za msingi 53 na Sekondari 14 zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya pikipiki hizo mbele ya viongozi wa ngazi ya Mkoa na wilaya, Bw Salum Mkuya kutoka idara ya Uratibu na Usimamizi wa Elimu TAMISEMI alisema kuwa pikipiki hizo zimeletwa ikiwa ni jitihada za serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini.
“Rais anadhamira ya dhati katika kuboresha elimu nchini alianza na elimumsingi bila malipo na juzi ameleta vitabu kwa ajili ya darasa la nne na sasa pikipiki kwa ajili ya kusimamia masuala ya elimu” alisema Mkuya
Bw Mkuya aliwataka waratibu kufanya kazi kwa juhudi na maarifa huku wakizingatia maadili ili kuongeza kiwango cha ufaulu katika wilaya ya Njombe kwa kuwa tayari nyenzo muhimu itakayowawezesha kusafiri maeneo mbalimbali kwa ajili ya ufuatiliaji wa elimu wanayo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Njombe , Ruth Msafiri aliwataka Waratibu Elimu Kata kutumia pikipiki hizo kwa kazi iliyokusudiwa huku akiagiza wale wote watakaotumia kinyume na madhumuni kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Ile dhana ya kuwa mali za serikali hazina mwenyewe muifute kabisa naomba mkavitunze vyombo hivi na mvitumie vizuri, msivigeuze kuwa bodaboda au vyombo vya kuendea shambani badala ya kufuatilia masuala ya elimu na mviendeshe kama watumishi wa umma” alisema Msafiri.
“Tunaishukuru serikali kwa kutuletea pikipiki hizi kwa ajili ya waratibu elimu Kata, tuliweza kufanya vizuri bila kuwa na nyenzo sasa tumepata nyenzo tutahakikisha ufaulu unakuwa kwa asilimia 100.”Aliongeza Msafiri.
Aliongeza kuwa uwepo wa vitendea kazi utaamsha na kuongeza hali ya uwajibikaji na maendeleo ya elimu katika Halmashauri ya wilaya ya Njombe.
Alibainisha kuwa wilaya ya Njombe imeweka utaratibu wa kufanya vikao mara mbili kwa mwaka vikiwa na lengo la kufanya tathimini ya masuala ya elimu pamoja na kufanya ziara za mara kwa mara kwenye Shule kufanya kaguzi mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya waratibu elimu Kata wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe baada ya kupewa pikipiki Bw. Neno Lulandala ambaye ni mratibu elimu Kata ya Kichiwa aliahidi kutumia vyombo hivyo kufuatilia maendeleo ya elimu ili kuinua kiwango cha ufaulu kwenye shule.
“Kwanza tunaishukuru serikali kwa kutupatia vyombo hivi ambavyo vitarahisisha sana ufuatiliaji wa masuala ya elimu kwenye shule za Sekondari na Msingi, kwa niaba ya wenzangu tunaahidi kutumia pikipiki hizi kwa madhumuni yaliyokusudiwa ili kuinua kiwango cha taaluma katika wilaya yetu” alisema Lulandala.
Halmashauri ya wilaya ya Njombe inajumla ya Kata 12 ambapo kila Kata ina mratibu elimu wake. Upande wa shule za Sekondari ziko 14 huku shule za serikali zikiwa 11 na binafsi zikiwa tatu. Upande wa shule za Msingi Halmashauri ya wilaya ya Njombe shule 53, shule za serikali zikiwa 52 na binafsi ikiwa moja.
Mwakilishi kutoka Idara ya Uratibu na Usimamizi wa Elimu ya TAMISEMI ,Salum Mkuya (watatu kutoka kushoto) akimkabidhi mkuu wa Wilaya ya Njombe Ruth Msafiri funguo za pikipiki kwa ajili ya waratibu elimu Kata wa Halmashauri ya willaya ya Njombe
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe , Frank Komba akimkabidhi Neno Lulandala mmoja ya waratibu elimu Kata funguo za Pikipiki zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya waratibu elimu Kata wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa