Kamati ya Ulinzi na usalama ya wilaya ya Njombe imejipanga kuwashughulikia na kuwathibiti wote ambao wanawapatia mimba watoto kama wanavyoshughulikiwa wezi wilayani hapa
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi Ruth Msafiri wakati akifungua kikao cha kufanya tathimini juu ya ukatili dhidi ya watoto kwa wadau mbalimbali Wilayani hapa wakiwemo madiwani, wakuu wa Idara na Vitengo, wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali ,vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na timu ya Ulinzi na usalama wa mtoto ya Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.
Akizungumza katika kikao hicho Bi Msafiri alisema kuwa jamii inapaswa kushiriki katika kuwalinda watoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao kwa kuwa watoto wa leo ni viongozi wa kesho. Aliongeza kuwa suala la kuwalinda watoto lazima yafanyike maamuzi magumu ambayo yatakuwa mfano kwa wale wote wenye tabia ya kufanya ukatili dhidi ya watoto.
Alisema kuwa wazazi na jamii lazima wajenge mazoea ya kukaa na watoto wa kike na kiume na kuwafundisha elimu ya kujitambua pamoja na wazazi kuhakikisha wanatoa taarifa na kuwafichua wanaofanya ukatili dhidi ya watoto katika maeneo yao.
“ Elimu kwa watoto wetu ni muhimu na vianzishwe kwa wingi vikundi vya TUSEME katika shule zetu ili vitumike katika kutoa elimu shuleni, tutapata taifa lisilokuwa na maendeleo endapo tutaruhusu watoto wapewe mimba” alisema Bi Msafiri.
Aliongeza kuwa endapo mtoto atapewa mimba wazazi watawajibika kutoa maelezo juu ya swala hilo huku akitaja kifo kuwa ni miongoni mwa athali za mimba za utotoni kwa watoto kutoka na via vya uzazi kutokomaa
Aliwataka wazazi kuhakikisha wanaendelea kuchangia chakula cha mchana kwenye Shule pamoja na kuwapatia lishe bora ikiwemo kuzingatia ushauri wa madaktari katika suala la unyonyeshaji wa watoto ili kupunguza hali ya udumavu kwa watoto.
Sambamba na hilo Bi Msafiri aliwataka madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kuhakikisha wanapopitisha bajeti suala la ulinzi na usalama wa watoto linapewa kipaumbele ili kuweza kutokomeza vitendo vya ukatili .
“Mtoto wa leo ni kiongozi wa kesho na mustakabali wa taifa letu hapo baadae hivyo hakikisheni bajeti ya wilaya inatenga fungu la kutosha linalolenga kuhudumia watoto katika Nyanja zote za makuzi ya mtoto ikiwemo chekechea na awali, mifumo ya ulinzi ngazi zote za Vijiji na Kata pamoja na ulinzi wa Kisheria.” Aliongeza Bi Msafiri.
Aidha, alipiga marufuku msemo wa mtoto wa mwenzio ni mkubwa mwenzio na kuahidi kuwachulia hatua wale wato wanaokwenda kinyume na maagizo ya Rais ikiwemo wanaopinga walipewa mimba kutoendelea na shule kama ilivyoagizwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli.
Hadi sasa Wilaya ya Njombe inajumla ya matukio 43 ya ukatili wa watoto ikiwemo matukio 26 ya ubakaji. Katika matukio hayo mashauri yaliyoisha yako tisa huku mashauri manne washitakiwa wamepewa adhabu ya kifungo na mashauri matano washitakiwa wameachiwa huru baada ya kukosekana kwa ushahidi na mashaidi.
Aidha, mashauri tisa yako katika hatua ya usikilizwaji, mashauri manne yako hatua ya kusoma hoja na mashauri 18 yapo katika hatua za kutajwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa