Jumla ya wanafunzi 2282 kutoka katika Halmashauri ya Wilaya Njombe watarajia kufanya mtihani wa Taifa wa kuhitimu elimu ya msingi unaotarajiwa kufanyika nchi nzima kuanzia Septemba 6 hadi 7 mwaka 2017.
Idadi hiyo inajumuisha wanafunzi wavulana 958 na wasichana 1324 kutoka shule 51 ambazo zinafanya mtihani katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.
Wanafunzi wanaofanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka huu ni wale walioanza darasa la kwanza mwaka 2011 na tayari Halmashauri imefanya maandalizi ya msingi ili kufanikisha ufanyikaji wa mtihani huu ikiwemo kutoa mafunzo kwa wasimamizi 150 ambao watasimamia mtihani huu.
Katika mtihani unaofanyika sasa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe inatarajia kufaulisha kwa zaidi ya asilimia 85 tofauti na mwaka jana ambapo ufaulu ulikuwa kwa asilimia 75.7
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe inatoa wito kwa wanafunzi wote kufanya maandalizi ya kutosha, kujiamini kwa kile walichosoma na kutofanya udanganyifu wa aina yoyote ile utakaopelekea kufutiwa matokeo yao na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Aidha, wazazi/walezi wanashauriwa kuwahamasisha watoto kufanya vizuri mitihani yao ambayo ni kwa manufaa ya maisha yao ya baadae. Sambamba na hilo wazazi wanatakiwa kuhakikisha wanatoa vifaa vyote muhimu kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi kufanya mitihani yao vizuri ikiwemo kalamu, rula, mkebe pamoja na vifaa vingine vinavyoruhusiwa katika mtihani.
Kwa upande wa mwaka jana jumla ya wanafunzi 1940 wavulana 849 na wasichana 1096 walifanya mtihani wa darasa la saba kutoka katika Halmashauri ya wilaya ya Njombe na ufaulu ulikuwa kwa asilima 75.7 na kufanya Halmashauri kushika nafasi ya 4 kwa mkoa wa Njombe.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe inajumla ya shule za Msingi 53 ambapo shule moja ni ya binafsi na shule 52 zikiwa za serikali. Katika mtihani unaofanyika mwaka huu shule mbili hazifanyi mtihani huo kutokana na kutokuwa na wanafunzi wa darasa la saba.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa