Kijiji cha Itipingi kilichopo katika Halmashauri ya wilaya ya Njombe kinatekeleza mradi wa upandaji wa miti ekari 30 wenye thamani ya shilingi 22,564,117.37kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini wilayani Njombe.
Mradi huu ni miongoni mwa miradi iliyobuniwa kwa ajili ya kutoa ajira za muda kwa walengwa waliopo katika mpango wa kunusuru kaya masikini.
Shamba hili limepandwa miche 19,500 aina ya milingoti ya kisasa ambapo kazi zote kuanzia kusafisha shamba, uchimbaji wa mashimo na upandaji wa miche ya miti zimefanywa na walengwa waliopo katika mpango wa kunusuru kaya masikini ikiwa ni sehemu ya ajira za muda kwa kaya masikini ili kuweza kuwaongezea kipato.
Kupitia mradi huu walengwa 173 walioshiriki katika maandalizi wamelipwa kiasi cha Tsh 13,604,500.00 na hivyo kujiongezea kipato.
Fedha hizi zimewawezesha baadhi kununua chakula,mifugo kwa ajili ya biashara na chakula, kuboresha makazi yao pamoja na kununua mbolea kwa ajili ya kuendesha kilimo.
Mbali na walengwa kunufaika kijiji cha Itipingi nacho kimenufaika kwa kuwa wao ndio wamiliki.
Aidha, uwepo wa miti hii unakihakikishia kijiji cha Itipingi kuwa na madawati ya kutosha ambayo yatapatikana kutokana na kupasua mbao pamoja na kupaua majengo mbalimbali ya serikali yatakayokuwa yanajengwa katika kijiji cha Itipingi au kuuza kama nguzo za umeme na mbao na kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na shughuli zingine za kimaendeleo.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa