Unapofika katika kijiji cha Image ambacho ni miongoni mwa vijiji vya mfano Tanzania katika utekelezaji wa kampeni ya afya na usafi wa mazingira, moja ya kivutio kikubwa ambacho ni kielelezo tosha cha mafanikio ya Kampeni ya Afya na usafi wa wa mazingira ni utunzaji wa mazingira katika shule ya Msingi Image iliyopo katika kijiji cha Image Kata ya Kidegembye katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.
Mbali na kuwepo na ndoo za kuzolea uchafu karibu kila baada ya mita kadhaa, shule hii imezungukwa na mabango yenye ujumbe wa aina mbalimbali unaosisitiza elimu na usafi wa mazingira.
Shule ya Msingi Image ambayo ilianzishwa mwaka 1974 mbali ya kuwa na vyoo bora vilivyozingatia mahitaji maalum kwa walemavu na wasichana waliopevuka, inamiundombinu ya kunawia mikono baada ya kutoka chooni.
Miundombinu hii imewafanya wanafunzi kutougua magonjwa yatokanayo na uchafu ambapo hapo awali kabla ya Kampeni ya afya na usafi wa mazingira idadi kubwa ya wanafunzi walikuwa wakikabiliwa nayo.
Shule hii ni miongoni mwa shule za msingi zinazotekeleza kampeni ya afya na usafi wa mazingira kupitia shirika la UNICEF pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.
Kupitia kampeni ya afya na usafi wa mazingira, kiwango cha ufaulu kimeongezeka kutokana na kuwepo kwa mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishia.
Kwa mujibu wa mkuu wa shule ya Image, Shadrack Sodike alisema kuwa ya kabla ya kampeni ya afya na usafi wa mazingira kiwango cha ufaulu kilikuwa kidogo kuliko sasa.
Alisema kuwa kampeni ya usafi wa mazingira imewezesha ujenzi wa vyoo bora jambo ambalo limechochea wanafunzi wengi kufika shuleni hususani wasichana kutokana na kutokuogopa na kuwepo na mazingira mazuri ya kuwasitiri wawapo katika hedhi hivyo kupata muda wa kusoma zaidi wa kujifunza tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
"Awali wanafunzi wa kike waliopevuka kila mwezi walikuwa wanakosa masomo wakati mwingine hadi wiki moja jambo lililochangia kuathili maendeleo yao kitaaluma, hii ilitokana na miundombinu kutokuwa rafiki hivyo kulazimika kushinda nyumbani, Sasa hakuna mwanafunzi wa kike anayekosa masomo kutokana na vyoo bora vilivyozingatia mahitaji yao ya kibaiolojia" anabainisha Sodike
"Kiwango cha ufaulu kimeongeza ambapo toka mwaka 2014 hatujawahi kushuka chini ya asilimia 80 huku mwaka 2015 na 2016 ufaulu ukiwa kwa asilimia 100" alibainisha Sodike
"Hapa tuna programu ya usafi wa mazingira shuleni (SWASH) wanafunzi wana kikundi chao ambacho kazi yake ni kutoa elimu kuhusu afya na usafi wa mazingira kwa wanafunzi wenzao kwa njia mbalimbali za nyimbo, ngojera na maigizo" aliongeza Sodike.
Unapokwenda kwenye vyoo vya shule hii ambavyo ni vya sinki huku sakafu yake ni marumaru unakutana na bango lenye ujumbe unaomkumbusha mwanafunzi nini anatakiwa kufanya kabla na baada ya kutoka chooni.
Kwa kuwa wanafunzi wanakula chakula cha mchana shuleni, kimetengwa chumba maalumu kwa ajili ya kuhifadhi maji safi na salama ili kulinda afya za wanafunzi.
Kampeni ya afya na usafi wa mazingira imeleta manufaa makubwa kwa wanafunzi wa Image.
Wanafunzi wa shule ya Msingi Image iliyopo wilayani Njombe wakiimba kabla ya kunawa mikono kwa ajili ya chakula cha mchana, Mbinu hii huwa wanaitumia ili kukumbushana umuhimu wa kunawa mikono kabla na baada ya kula pia wakati wa kutoka chooni.
Moja ya mabango yaliyo na ujumbe unaomkumbusha mwanafunzi vitu anavyotakiwa kuvifanya wakati akiingia chooni na baada ya kutoka choo katika shule ya Msingi Image iliyopo wilayani Njombe
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa