Katika kutambua umuhimu wa kutoa elimu kwa njia ya vielelezo na kutunza mazingira Halmashauri ya wilaya ya Njombe, imeanzisha kitalu cha miche ya miti katika kijiji cha Lunguya kilichopo Kata ya Mtwango wilayani Njombe.
Hadi sasa jumla ya miche ya miti aina ya mikalatusi 16,920 tayari imependwa katika kitalu hicho na inasimamiwa na wataalamu kutoka katika Halmashauri.
Kuwepo kwa kitalu hiki kunaongeza wigo wa utoaji wa elimu ya ugani-misitu kwa vitendo katika maeneo ya Halmashauri ya wilaya pamoja na kuongeza kasi ya utunzaji wa mazingira.
Halmashauri imeanzisha kitalu hiki ikiwa ni moja ya mkakati wa uwekezaji ili kuiongezea mapato pamoja na kuongeza nguvu ya kuzisaidia taasisi za elimu kukabiliana na uhaba wa madawati na vikundi mbalimbali vyenye mahitaji maalum ya kuanzisha mashamba ya miti.
Msimu huu wa mvua Halmashauri itasambaza miche 1000 kwenye kila Kata kwa ajili ya kuigawa kwenye kila shule ili iweze kutumika kutengenezea madawati na meza hapo baadae pamoja na taasisi mbalimbali za Umma kwenye maeneo ya Kata.
Sambamba na hilo Halmashauri inatarajia kusambaza miche iliyooteshwa kwa vikundi vya kijamii ikiwemo yatima, vijana na wanawake ili kuongeza nguvu ya kipato kwa makundi mbalimbali na mingine itauzwa kwa ajili ya kuongeza mapato.
Katika kuhakikisha kuwa mpango huu unakuwa endelevu Halmashauri ya Wilaya ya Njombe imeweka mikakati ya kupanua wigo wa uoteshaji wa miche ya miti kwa kuongeza ukubwa wa kitalu pamoja na kufanya mipango ya kuanzisha kitalu kingine katika Kata ya Matembwe.
Halmashauri inatarajia kupanua wigo wa aina ya miche inayooteshwa ikiwemo ile inayokuwa haraka pamoja na miti rafiki ya maji kwa ajili ya kupanda kwenye vyanzo vya maji,miche ya matunda, mapambo , kivuli na mazao mengine ya misitu.
Aidha, Halmashauri inatarajia kuanzisha shamba la miti lenye zaidi ya hekari 1000 katika kijiji cha nyave ikiwa ni sehemu ya uwekezaji wa Halmashauri katika sekta ya misitu.
Tangu kuanzishwa kwa kitalu hiki wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Halmashauri wamekuwa wakijitokeza kwa nyakati tofauti kupata elimu ya uanzishaji wa kitalu cha miti, usimamizi na uendeshaji, elimu ambayo inatolea bure kwa wananchi wote.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa