Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dr Hamis Kigwangalla, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kwa kuboresha huduma katika kituo cha afya Lupembe baada ya kukarabati chumba cha upasuaji na jengo la mama na mtoto.
Pongezi hizo zimetolewa wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ambapo alikagua kituo cha Afya Lupembe na Kichiwa ambapo katika kituo cha Afya Lupembe huduma ya upasuaji inatarajiwa kuanza muda wowote.
Akizungumza na wananchi katika Kata ya Lupembe na Kichiwa mara baada ya kuweka jiwe la Msingi katika jengo la mama na mtoto katika kituo cha afya Lupembe, Dr .Kigwangalla alisema kuwa ameridhishwa na namna Halmashauri inavyotekeleza maagizo ya Serikali ikiwemo agizo la kila kituo cha Afya kuanzisha huduma za upasuaji agizo lililotolewa wilayani Meatu.
"Mimi ni mgumu sana kutoa pongezi na kwenye ziara zangu huwa sicheki, siwezi kucheka wakati wakinamama na watoto wanakufa, lakini panapofanyika mambo mazuri lazima tupongeze, hongereni sana kwa kuboresha huduma katika kituo cha afya Lupembe hasa chumba cha upasuaji, hongereni sana ." alisema Dr Kigwagalla.
"Huduma zinazotolewa hapa ni za kiwango cha hospitali ya Wilaya au Mkoa msione majengo yaliyo mkadharau ,kitaalamu tunaangalia huduma zinazotolewa . Uboreshaji huu utasaidia kupunguza vifo vya akinamama na watoto kutokana na kupunguza umbali wa kupata huduma za upasuaji maana nasikia zamani mlikuwa mnakwenda Hospitali ya Mkoa Kibena ambapo ni zaidi ya kilometa 60, sasa huduma zitapatikana hapa hapa" aliongeza Dr Kigwagalla.
Dr kigwangalla alieleza kuwa serikali imeongeza mgao wa dawa na kuitaka Halmashauri kuhakikisha inasimamia vizuri dawa zote zinazoletwa na kuwachukulia hatua wale wenye kukiuka maagizo ya Serikali.
Akijibu ombi la wananchi wa Kichiwa la kupatiwa gari la wagonjwa kwa ajili ya kituo cha afya, Dr kigwagala alisema kuwa suala hilo atalifanyia kazi na pindi fursa itakapopatikana Halmashauri ya wilaya ya Njombe itapewa kipaumbele.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Lupembe lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Bw. Joram Isamil Hongoli aliiomba Serikali kupitia Naibu Waziri, Dr Kigwangalla kusaidia upatikanaji wa mashine za X-ray , Utra Sound pamoja na vifaa vingine muhimu katika vituo vya afya vya Halmashauri ya wilaya ya Njombe.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe imeendelea kutekeleza sera ya kuwa na kituo cha afya katika kila Kata na zahanati katika kila kijiji kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi pamoja na kuwahamasisha wananchi kuanza ujenzi wa vituo vya huduma katika maeneo ambayo hayana.
Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe imetenga shilingi 276,420,522 kupitia vyanzo vya mapato ya ndani na ruzuku kutoka serikali kuu kwa ajili ya kukamilisha maboma matano ya zahanati na kuanza ujenzi wa majengo ya upasuaji katika vituo vya afya vya Mtwango na Kichiwa ambapo vimetengewa shilingi milioni 70 pamoja na kuanza kwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa