Halmashauri ya Wilaya ya Njombe imesaini mkataba wenye thamani ya zaidi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa umwagiliaji katika kijiji cha Itipingi kilichopo Kata ya Igongolo Wilayani Njombe,
Mradi huo unafadhiliwa na Shirika la JAICA kutoka nchini Japani ambao utekelezaji wake unaanza januari mwaka huu, utajengwa na mkandalasi Engineering Plus kutoka Dar es Salaama na utatekelezwa kwa kipindi cha miezi nane huku ukisimamiwa kwa pamoja baina ya wataalamu wa umwagiliaji kutoka kanda ya Mbeya na wa Halmashauri ya Njombe.
Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mkataba huo uliohudhuriwa na meneja uendeshaji wa kampuni ya Engineering Plus, wawakilishi wa kikundi cha umwagiliaji skimu ya Itipingi, wataalamu kutoka ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe , Bi Monica PZ Kwiluhya, amewataka wakandalasi kutekeleza mradi huu kwa wakati na ubora unakubalika.
“Kawaida mimi huwa siongezi muda wa kutekeleza mradi kwa kuwa pesa tayari ipo hivyo hakuna visingizio, siko tayari kuona mradi unacheleweshwa pasipokuwa na sababu za msingi maana pesa hizi ni za wafadhili na mradi ukicheleweshwa zinatakiwa zirudi” alisema Kwiluhya.
Amewataka wakandalasi kushirikiana na wananchi kwa kazi zile ambazo zinaweza kufanywa na wananchi pamoja na kujiepusha na vitendo vitakavyopelekea kukosa ushirikiano kutoka kwa wananchi ambao ndio wamiliki wa mradi..
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe Bw. Valentino Hongoli amewataka wakandalasi kufanya kazi kwa mujibu wa makubaliano ya Mkataba kwa kuzingatia tarehe ya kuanza utekelezaji na tarehe ya kumaliza.
“Naomba mfanye kazi kwa kuzingatia thamani ya fedha na kwa viwango vinavyokubalika ili kuweza kutoa mtokeo chanya kwa wananchi” alisema Hongoli.
Kusainiwa kwa mkataba huu kunatoa matumaini kwa wananchi wa Itipingi ambapo awali walikuwa wakitumia mifereji katika kufanya kilimo cha uzalishaji wa mazao mbalimbali ikiwemo chakula na mboga mboga.
Mradi ukikamilika unatarajia kuwanufaisha zaidi ya wakazi 1500 ambao watakuwa wakilima mazao ikiwemo, mahindi, nyanya, vitunguu pamoja na mboga mboga. Mradi huu umekuja wakati muafaka ambapo Halmashauri iko katika hatua za mwisho kukamilisha kituo cha kuzuia upotevu wa mazao ya mboga mboga na matunda ili kuyaongeza thamani ambacho kimejengwa kwa ufadhili wa shirika la MIVARAF mjini Njombe.
Sambamba na hilo mradi huu ukikamilika utasaidia kuinua kipato cha wakulima, kuongeza lishe kwa jamii pamoja na kuiongezea Halmashauri Mapato.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa