Katika kuhakikisha mradi wa umwagiliaji katika kijiji cha Itipingi unatumika kama ilivyotarajiwa na kutoa matokeo chanya kwa wakulima , Halmashauri ya Wilaya ya Njombe imetoa elimu juu ya matumizi bora ya mradi huo wilayani hapa.
Mradi huu ambao ni miongoni mwa miradi mikubwa ya umwagiliaji Wilayani Njombe ,hadi kukamilika kwake umegharimu zaidi ya Milioni 300 ukiwa na mfereji wa umwagiliaji wenye urefu wa mita 1725 na utawahudumia zaidi ya wakulima 1500 kutoka katika kijiji cha itipingi pamoja na maeneo ya jirani.
Mradi huu unaeneo la umwagilia la hekari 160 ambapo hadi sasa hekari zaidi ya 80 zinatumika na hekari 40 tayari zimelimwa na kupandwa mazao mbalimbali ikiwemo mboga mboga ambazo zinawahakikishia wakulima na wananchi kipato pamoja na chakula bora.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara baina ya wataalamu wa Halmashauri pamoja na wanakijiji cha Itipingi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe , Monica Kwiluhya alisema kuwa baada ya kukamilika kwa mradi huo anatarajia kilimo cha kisasa kiendeshwe pamoja na kuulinda mradi ili uweze kutoa manufaa kwa kipindi kirefu.
Alisema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe baada ya kukabidhiwa mradi huo imejipanga kuhakikisha mradi unatumika kadiri ulivyopangwa na kutoa manufaa kwa wakazi wa kijiji cha Itipingi.
“ Leo nimekuja na wataalaumu wote ili waweze kutoa ufafanuzi wa namna mradi huu unavyotakiwa kutumika ili uweze kudumu na mpate mazao bora, pamoja na kulinda maji ili yaendelee kuwepo kwa vizazi vya leo” alisema Kwiluhya.
Aliwataka vijana kujiunga katika vikundi na kuomba mikopo kwenye Halmashauri kwa ajili ya kuendesha kilimo hali itakayowawezesha kupata kipato na kujikwamua kiuchumi.
Kupitia mkutano huu wananchi walielezwa namna bora ya utunzaji wa vyanzo vya maji ikiwemo kupanda miti rafiki ya maji, kutokulima kwenye vyanzo vya maji pamoja na kutokupeleka mifugo kwenye vyanzo vya maji na kupitisha mifugo yao kwenye mfereji jambo ambalo litapelekea migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
“Ili kuondoa migogoro baina ya wakulima na wafugaji , Nimekuja na wataalamu wa mifugo kwa ajili ya kaangalia eneo la kujenga mabirika ya kunyweshea mifugo ili kuepusha mifugo kuingia kwenye mashamba ya wakulima” alisema Kwiluhya.
Katika mkutano huo wananchi walifundishwa namna ya kuweka akiba ili kuweza kukarabati mradi pindi unapoharibika pamoja na kanuni za kilimo bora ili kuwawezesha kupata mazao mengi yaliyo bora.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa