Naibu Waziri wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Aloyce Kamwelwe, ameweka jiwe la Msingi katika mradi wa maji Kijiji cha Iwafi kilichopo katika Halmashauri ya wilaya ya Njombe.
Uwekaji huo wa jiwe la msingi umefanywa na naibu waziri Kamwelwe wakati akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maji inayotekelezwa katika Halmashauri ya wilaya ya Njombe.
Mradi huo maji kijiji cha Iwafi ambao umewekewa jiwe la msingi hadi kukamilika kwake utagharimu zaidi ya Milioni 230 na utahudumia vitongoji sita kati ya vitongoji tisa vilivyopo katika kijiji cha Iwafi Kata ya Idamba. Sambamba na kuhudumia vijiji hivyo mradi huo utawanufaisha wakazi 2,514 ikiwemo wanafunzi 557 wa shule ya Msingi Iwafi na 259 wa shule ya sekondari Idamba.
Akizungumza katika mkutano wa Hadhara na wananchi katika kijiji cha Iwafi kata ya Idamba wilayani Njombe Mhandisi Kamwelwe aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maji na kuwataka wananchi kuhakikisha wanaitunza miradi hiyo.
“Nimeridhishwa na matumizi yenu ya fedha pamoja na utekelezaji wa miradi ya maji, nawapongeza sana endapo mtaendelea kutumia fedha hivi mwaka ujao tutawaongezeeni” alisema Mhandisi Kamwelwe.
“ Kutokana na miradi ya kutumia mashine za diesel kuwa na gharama kubwa nawashauri wakati mwingine mtumie umeme wa nguvu za jua japo najua huku kuna baadhi ya maeneo yana changamoto ya hali ya hewa” aliongeza Mhandisi Kamwelwe.
Mradi maji katika kijiji cha Iwafi unatekelezwa kwa pamoja baina ya shirika la Peoples’ Development Forum (PDF) kwa ushirikiano wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe na wananchi wa kijiji cha Iwafi kupitia programu ya mradi wa Maji, Afya na Usafi wa mazingira unaofadhiliwa na shirika la UNICEF.
Kazi ambazo zimekamilika hadi sasa katika mradi huu ambao utaendeshwa kwa mashine ya mafuta ya diesel kusukuma maji ni pamoja na ujenzi wa tanki lakukusanyia maji kwenye chanzo, ufungaji wa mashine ya kusukumia maji, uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa mabomba kwenye eneo lenye urefu wa mita 11934.
Upande wa ujenzi wa tanki la kutawanya maji kwenye vitongoji sita lenye ujazo wa lita elfu 50 upo katika hatua ya ukamilishaji na linatarajiwa kukamilika hivi karibuni na kuanza kutoa huduma kwenye kijiji cha Iwafi.
Katika kufanikisha mradi huu jamii imechangia nguvu kazi ikiwemo uchimbaji wa mitaro, kulaza mabomba na kuyafukia , usombaji wa mawe , ufyatuaji wa tofari ambavyo vyote kwa pamoja vina thamani zaidi ya milioni 25. Michango mingine inatoka kwa UNICEF na PDF ambao wanachangia zaidi ya milioni 155 na Halmashauri ya wilaya ya Njombe wanachangia zaidi ya milioni 50.
Akiwa katika ziara ya siku moja katika halmashauri ya wilaya ya Njombe Mhandishi Kamwelwe alikagua vituo vya maji vilivyofungwa mita katika eneo la Lupembe barazani ikiwa ni ufuatiliaji wa agizo la Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa ambalo alilitoa alipokuwepo katika ziara wilayani Njombe. Aidha, alipata nafasi ya kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo ya Iwafi na Lupembe na kutolea ufafanuzi masuala mbalimbali yaliyoulizwa na wananchi.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa