Halmashauri ya Wilaya ya Njombe imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 61 kwa vikundi vya wanawake na vijana ikiwa na lengo la kuongeza kipato na kuwainua kiuchumi.
Mikopo hiyo ambayo imetolewa kwa awamu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2017/2018 kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana (YDF) na ule wa wanawake (WDF) umevinufaisha vikundi 52 vya vijana na wanawake wilayani Hapa.
Kupitia mikopo hiyo vikundi 35 vya wanawake vimepewa mkopo wenye thamani ya shilingi milioni 40 huku upande wa vijana vikundi 17 vikipewa milioni 21.
Mikopo iliyotolewa imetokana na fedha ya bakaa ya mwaka 2016/2017 kiasi cha shilingi milioni 28, marejesho ya mikopo iliyotolewa awali kiasi cha milioni 25 huku mchango wa Halmashauri unaotokana na mapato ya ndani kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba 2017/2018 ukiwa ni milioni 13.
Mikopo hii imepitishiwa katika vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) vilivyo jirani na walengwa kwa lengo la kurahisisha zoezi la ukopeshaji na urejeshaji ikiwa ni pamoja na kuwapunguzia wakopaji gharama za ufuatiliaji wa mikopo Makao makuu ya wilaya Njombe Mjini.
Upitishaji huu wa mikopo kwenye SACCOS una lengo la kuipunguzia Halmashauri gharama za ufuatiliaji wa madeni hayo pamoja na kuwawezesha Vijana na Wanawake kujenga tabia ya kuweka akiba na kukopa katika SACCOS zilizo jirani nao badala ya kutegemea Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Wanawake tu.
Akizungumza na vikundi vya wanawake na vijana wakati wa kukabidhiwa hundi za mikopo hiyo Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Bi Ruth Msafiri ambaye alikua mgeni rasmi alivitaka vikundi vilivyopewa mikopo kuitumia vizuri ili kuweza kujikwambua kiuchumi.
“Naomba mkatumie mikopo hii kwa malengo mliyokusudia na miradi iliyopitishwa na wataalamu kwa kuwa serikali inatoa mikopo hii kwa riba ndogo kwa lengo la kuwainua kiuchumi, mkumbuke kuwa hii sio zawadi lazima irudishwe ili na wenzenu waweze kupewa” alisema Msafiri.
Aliwataka maafisa ugani wilayani hapa kuvisaidia vikundi vya kilimo na ufugaji kuendesha shughuli zao kisasa pamoja na kuacha kufanya biashara kwa mazoea ili malengo ya mikopo hiyo yaweze kutiamia.
Awali akisoma taarifa ya mfuko wa wanawake na vijana Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Bi Monica Kwiluhya alisema mikopo inayotolewa imeweza kuongeza mitaji ya shughuli na miradi ya vikundi ikiwemo kilimo cha mazao mbalimbali, Ufugaji wa mifugo , Ushonaji nguo, migahawa na vitalu vya miche ya miti mbalimbali.
“Kupitia Mifuko hii vijana na wanawake wameweza kuunganishwa na taasisi mbalimbali za kifedha kama vile SACCOS, VICOBA na benki ya Wananchi Njombe (NJOCOBA)” alisema Kwiluhya
Akizungumzia changamoto zinazoikabili Halmashauri katika utoaji wa mikopo hiyo alisema kuwa baadhi ya wanakikundi hutumia mkopo kinyume na miradi waliyoiombea, hivyo miradi hiyo hushindwa kuwa na tija na hatimaye hushindwa kurejesha mikopo kwa wakati.
Kuhusu ufumbuzi wa changamoto hiyo Kwiluhya alisema kuwa kabla ya vikundi kupewa mikopo Halmashauri inavijengea uwezo kwa kuvipatia elimu ya ujasiriamali pamoja na umuhimu wa kujiunga na SACCOS kwa lengo la kupata fursa nyingine ya kuweka akiba na kukopa ili waweze kuzalisha zaidi.
Mikopo inayotolewa ina lengo la kuwaongezea mitaji Vijana na Wanawake na Riba yake ni 10%. Tangu mwaka 2006 hadi sasa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe imetoa mikopo yenye zaidi ya shilingi milioni 561 kwa vikundi vya vijana na wanawake ambapo zaidi ya milioni 160 zimetolewa kwa vikundi 168 vya vijana na zaidi ya milioni 401 kwa vikundi 507 Vya wanawake.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa