Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Njombe limeridhia ufafanuzi uliotolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Monica Kwiluhya baada ya kumwagiza kutoa ufafanuzi kuhusu utumwaji wa fedha za asilimia 12 kwenye maeneo ya vijiji ambao ulikuwa haujafanyika kwa wakati .
Hali hii ilitokea wakati wa kufungua mkutano wa baraza la madiwani ambapo hufanyika kwa siku mbili huku siku ya kwanza ikiwa ni maalumu kwa kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali kwenye maeneo ya Kata ambazo uwasilishwa na diwani wa Kata husika.
Kufuatia kuchelewa kutumwa kwa asilimia hizo kwenye Kata madiwani walitaka ufafanuzi kutoka kwa mkurugenzi wa sababu zilizopeleka jambo hilo ambapo mkurugenzi pamoja na wataalamu walitoa ufafanuzi kuwa changamoto kubwa ni suala la mtandao
Hali hiyo ilipelekea baraza hilo kujigeuza kama kamati ambapo walimwagiza Mkurugenzi kuandaa taarifa ya kiasi kinachodaiwa kwenye kila Kata pamoja na sababau zilizopeleka kuchelewa kutumwa kwa asilimia hizo.
Akitoa ufafanuzi siku ya pili ya mkutano wa baraza la madiwani , Kwiluhya alisema kuwa sababu iliyopelekea kuchelewa kulipwa kwa asilimia hizo ni matatizo ya mfumo wa kupokelea mapato kuanzia mwezi Julai hadi Octoba hali iliyopelekea Halmashauri kushindwa kurudisha asilimia hizo kwa wakati.
“Mheshimiwa mwenyekiti kutokana na tatizo la mfumo Halmashauri iliwasiliana na ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Njombe pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tukiomba kutatuliwa kwa changamoto hii ili Halmashauri kutekeleza majukumu yake” alisema Bi Kwiluhya.
“Tayari katibu mkuu ameleta wataalam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kushughulikia changamoto hizi wakisaidiana na wataalam wetu na kwa sasa tatizo limeanza kupungua na malipo yameandaliwa” Aliongeza Kwiluhya.
Alifafanua kuwa kilichochelewesha kulipwa kwa asilimia hizo ni usuluhishi wa fedha kati ya mashine za kukusanyia mapato na taarifa ya mapato yanayosomeka katika mfumo kwenye ofisi kuu ya Halmashauri na kutaja kiasi kinachodaiwa na vijiji kuwa ni milioni 32 ikiwa ni fedha ya Mwezi Machi hadi June 2017.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo alisema kuwa Halmashauri kwa sasa imefanya mawasiliano na wamiliki wote wa simu za kukusanyia mapato kutoa ripoti ya kila siku ili kurahisisha usuluhisho wa miamala kati ya Halmashauri na wakusanyaji wakati wa uwasilishaji wa mapato jambo litakalosaidia upelekeaji wa asilimia hizo kwa wakati.
Mwaka wa fedha 2017/2018 katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe asilimia 12 za mwezi Julai na Agosti zimeshalipwa huku ile ya mwezi septemba yenye kiasi cha 10,953,936 hundi imeandaliwa kwa malipo.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa