Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Geita na wataalamu wa Halmashauri hiyo wamezipongeza SACCOS Zilizoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kutokana na ubunifu na utendaji mzuri wa kazi kwa kushirikiana na Halmashauri katika kuwakwamua wanawake na vijana wilayani Njombe.
Pongezi hizo zimetolewa wakati wa ziara waliyoifanya katika Halmashauri ya wilaya ya Njombe ikiwa na lengo la kujifunza namna mifuko ya wanawake na vijana inavyofanya kazi katika Halmashauri hii.
Akizungumza katika ziara hiyo mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Geita ,Bw. Elisha Lupuga alisema kuwa wamejifunza kitu kikubwa ambacho wanakwenda kukifanyia kazi katika Halmashauri yao.
"Kiukweli safari yetu imekuwa na manufaa makubwa kwani tumejifunza mambo mengi mazuri, tumepata elimu na tukitoka hapa tunakwenda kufanya mambo makubwa huko kwetu na tutawaalika mje kuona baada ya muda mfupi, sisi kule tuna majimbo mawili hivyo tunaweza kuanza na SACCOS moja kwa kila jimbo " alisema Bw. Lupuga.
"Hongereni sana SACCOS zenu ziko kama benki tu kwa muonekano pamoja na huduma zinazotolewa, hakika somo limeingia" aliongeza Bw. Lupuga.
Awali akisoma taarifa kuhusu namna mfuko wa wanawake na vijana unavyofanya kazi katika Halmashauri ya Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Bi Monica P.Z Kwiluhya, alieleza kuwa toka mwaka 2006 hadi 2017 Halmashauri imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani zaidi ya Milioni 400 kwa vikundi zaidi ya 500 vya wanawake na vijana.
Aliongeza kuwa mikopo hii hutolewa kupitia SACCOS zilizo jirani na walengwa kwa lengo la kurahishisha zoezi zima la ukopeshaji na urejeshaji ikiwa ni pamoja na kuwapunguzia gharama za ufuatiliaji wilayani wakopaji na kuipunguzia gharama Halmashauri za ufuatiliaji wa madeni hayo pamoja na kuwajengea vijana na wanawake tabia ya kuweka akiba na kukopa katika SACCOS zilizo jirani nao badala ya kutegemea mfuko wa maendeleo ya vijana tu.
Alieleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri imekopesha jumla ya shilingi Milioni 114,500,000 kwa vikundi 88 huku vikundi vya wanawake vikiwa 61 na kupata Milioni 68 na vijana vikundi 27 vikipata 46 milioni huku mchango wa Halmashauri ukiwa zaidi ya milioni 80 ambazo ni sawa na zaidi ya asilimia 82 ya fedha zilizokisiwa kuchangwa kupitia mapato ya ndani.
Kuhusu mafanikio ambayo yametokana na na mikopo inayotolewa kwa vikundi vya vijana na wanawake watanowatano kwa lengo la kuzikwamua familia Bi Kwiluhya alisema kuwa wanavikundi wengi wameongeza mitaji yao na kupanua shughuli wanazofanya ikiwemo kilimo, ufugaji wa mifugo mbalimbali , ushonaji nguo, migahawa ,kulipa ada pamoja na kuboresha makazi.
" Halmashauri imeweza kuviunganisha vikundi vya vijana na wanawake na taasisi mbalimbali za kifedha kama vile SACCOS, VIKOBA, Benki ya wananchi Njombe pamoja na taasisi nyingine" aliongeza Bi Kwiluhya.
Katika ziara hiyo madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita pamoja na watalumu wa Wilaya hiyo walitembelea SACCOS ya Nyombo iliyopo katika kijiji cha Nyombo kata ya Ikuna ,SACCOS ya Ibumila iliyopoa Kijiji cha Ibumila Kata ya Kichiwa Pamoja na kikundi cha Ushonaji Nguo Nyombo kilichopo kijiji cha Nyombo.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ina jumla ya SACCOS 12 na mikopo ya wanawake na vijana inalengo la kuwainua vijana na wanawake kiuchumi pamoja na kuwaongezea mitaji huku liba yake ikiwa ni asilimia 10 tu
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa