Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Joseph Magufuli ametoa msaada wa vitanda, mashuka na magodoro kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za afya katika Halmashauri ya wilaya ya Njombe.
Msaada uliotolewa ni pamoja na vitanda 20 vya kulalia wagonjwa, magodoro 20, vitanda 5 kwa ajili ya kujifungulia wakinamama wajawazito pamoja na mashuka 50 ambayo yatasaida kuboresha mazingira ya wagonjwa wanapolala wakati wakipatiwa huduma za afya.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Bi Monica Kwiluhya amemshukuru Rais Magufuli kwa msaada huo ambao utaboresha utoaji wa huduma za afya kwenye Halmashauri.
“Msaada huu umekuja wakati muafaka na kwaniaba ya Halmashauri napenda kutoa shukrani kwa mheshimiwa rais Magufuli, aidha Halmashauri imefanya mgao huo wa vifaa tiba kwa kuzingatia maeneo yenye uhaba mkubwa na maeneo yenye mzigo mkubwa wa wagonjwa.” Alisema Bi Kwiluhya.
“Halmashauri kwenye mipango yetu inaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kupunguza tatizo la vifaa tiba ingawa hatuna upungufu mkubwa na kwa sasa tuko kwenye bajeti tunatarajia kuweka ujenzi wa hospitali ili kuboresha huduma za afya hivyo tunahitaji wahisani wengine waweze kutusaidia vifaa tiba.” aliongeza Kwiluhya.
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Lupembe lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi Ruth Msafiri katika makabidhiano hayo alisema anamshukuru Rais kwa kutimiza ahadi aliyoitoa kwa wabunge ya kusaidia sekta ya afya nchini.
“Msaada huu umekuja wakati muafaka na ninaomba wananchi wamuunge mkono mkuu wan chi, kama unataka kutoa sadaka yenye thawabu basi changia huduma za afya ili kuweza kuokoa maisha ya watu wengi” alisema Hongoli.
“Tumeanzisha huduma za upasuaji wakinamama wajawazito katika kituo cha afya Lupembe msaada huu utasidia sana kupunguza tatizo la vifaa tiba katika kituo hicho kwani sasa kinapata wagonjwa wengi ambao zamani walikuwa wanalazimika kusafiri umbali wa takribani kilometa 60 kwa ajili ya kufuata huduma hii.”
Kabla ya msaada huu mahitaji ya vitanda katika vituo 27 vya kutolea huduma za afya vilivyopo katika Halmashauri ya wilaya ya Njombe yalikuwa ni 91 huku vitanda 71 vikiwepo hivyo kufanya upungufu wa vitanda 20 kwa sasa. Upande wa vitanda vya kujifungulia mahitaji ni 46 vilivyopo sasa baada ya msaada ni 36 na kuwa na upungufu wa vitanda 50.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa