Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka ameipongeza Halmashauri ya Wilaya Njombe kwa kupata hati safi katika hesabu za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Pongezi hizo alizitoa katika baraza maalumu la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Njombe la kujadili taarifa na mpango kazi wa hoja za Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali lililofanyika wilayani Njombe.
Akizungumza katika baraza hilo Ole Sendeka alisema kuwa anaipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kwa kupata hati safi kwa mahesabu ya jumla na hati zinazoridhisha kwa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kwa kipindi cha mwaka 2016/2017.
“Nitoe pongezi za dhati kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Baraza la M
adiwani, Mkurugenzi Mtendaji pamoja na wataalamu wake kwa kazi nzuri mnazofanya. Katika mkoa wangu kuna Halmashauri sita, tano zimepokea hati safi na moja hati yenye mashaka kwenye hesabu za serikali katika mwaka wa fedha 2015/2016 na nyinyi ni miongoni mwa halmashauri zilizopata hati safi". Alisema Ole Sendeka.
“Miradi yenu inakidhi viwango kwani niliitembelea na kuiona katika ziara yangu nilioifanya katika Halmashauri yenu, naomba kila mtu ajue namna ya kuitumia nafasi yake kama mtumishi wa Umma, kuimarisha mifumo ya ndani ya mapato na usimamizi ili kuzidi kuboresha na kuendeleza miradi” aliongeza Ole Sendeke
Alizitaka halmashauri kuendeleza uwazi na uwajibikaji kwa kufuata matumizi sahihi ya fedha kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na serikali.
“Uwazi na uwajibikaji ni mkataba wetu na wananchi kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, Sehemu nyingine nimewasimamisha kazi watumishi, bora kuwa na watumishi wachache wachapakazi kuliko watumishi wengi wasiofanya kazi, lakini kwa upande wenu mnafanya kazi nzuri na ninafurahi na kuwapongeza sana” alisema Ole Sendeka
Awali akifungua baraza maalumu la Madiwani Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Bw Valentino Aidan Hongoli alisema kuwa Halmashauri imepata hati safi kwa hesabu za jumla pamoja na kupata hati zinazoridhisha katika miradi ya maendeleo ikiwemo barabara, maji, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ,kilimo na mifugo pamoja na mfuko wa pamoja wa afya (Health basket fund).
Aliongeza kuwa Halmashauri imejipanga kuhakikisha kuwa inafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuyawekea mipango na kuitekeleza kwa mafanikio ambayo yataleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo.
Mwaka wa 2015/2016 katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe zilitolewa hoja 51 na hoja 22 za miaka ya nyuma. Kati ya hoja 38 zimehakikiwa na mkaguzi na kufungwa sawa na asilimia 74.51 ,hoja 13 zipo katika hatua ya utekelezaji sawa 25.49%. Hoja 12 kati ya zile 22 za miaka ya nyuma zimeakikiwa na kufungwa na hoja 10 zinazosalia ni zile ambazo zipo katika hatua za utekelezaji.
Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe imejipanga kuhakikisha enaendelea kupata hati safi na kufanya vizuri katika nyanja mbalimbali ili kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa