Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe umefanya mkutano wa hadhara katika Kata ya Lupembe ikiwa ni utaratibu ulioanzishwa kwa lengo la kupokea na kusikiliza Kero na changamoto mbalimbali zilizopo katika Kata zake.
Katika mkutano huo ambao ulimjumuisha mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe , Valentino Hongoli, Mkurugenzi mtendaji Monica Kwiluhya pamoja na wataalamu kutoka katika ngazi ya Halmashauri, Kata na Kijiji cha Lupembe ambapo wananchi walipata fursa ya kuuliza maswali katika maswala mtambuka pamoja na kutoa changamoto zinazowakabili katika kata yao.
Akijibu changamoto ya wodi la kina mama katika kituo cha afya Lupembe ambalo bado halijakamilika, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe, Monica Kwiluhya aliahidi hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu wodi hiyo itakuwa imekamilika na kuanza kutumika.
“Halmashauri inafanya jitihada kubwa kuhakikisha wodi ya kinamama inakamilika nawahakikishia wodi hii itakamilika mwaka huu na nyinyi wenyewe ni mashahidi kwa kazi kubwa tuliyoifanya katika kituo chenu, Naomba tushirikiane kujenga shimo la maji machafu” alisema Kwiluhya
“Halmashauri inafanya mpango wa kupata jenereta kwa ajili ya chumba cha upasuaji katika kituo cha afya Lupembe ambapo upasuaji umeanza kufanyika, Tumepoteza wakinamama na watoto wengi sasa huduma ya upasuaji imeanza tunaomba mkawe mabalozi wazuri na kukitumia vizuri kituo chenu” aliongeza Kwiluhya.
Akizungumzia changamoto ya maji na miundombinu yake katika Kata ya Lupembe alisema kuwa tayari jumuiya ya watumia maji imeshaundwa na inafanya kazi. Alisema kuwa wataalamu wa Halmashauri wamepita kufanya upembezi kwa ajili ya kuweka katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 ili kuboresha miundombinu ya maji na kuweza kukidhi mahitaji katika kata ya Lupembe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Valentino Hongoli aliwataka wananchi wa Lupembe kushiriki katika maendeleo na kutoitegemea serikali pekee katika kutekeleza mira kwenye maeneo yao.
“Tunaomba mtoe ushirikiano na wataalumu waliopo katika Kata hii kuweza kutatua matatizo yaliyopo ndani ya uwezo wenu badala ya kusubili serikali, kufanya hivyo tutakuwa tunachelewesha maendeleo katika Kata yetu.” alisema Hongoli.
Kupitia mkutano huo wananchi wa Kata ya Lupembe wameishukuru Halmashuri ya Wilaya ya Njombe kwa kuanzisha huduma ya upasuaji kwa akina mama wajawazito katika kituo cha afya Lupembe ambapo hadi kufikia ijumaa ya wiki iliyopita akina mama tisa walikuwa wamekwisha fanyiwa upasuaji na wanaendelea vizuri.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa