Halmashauri ya Wilaya ya Njombe inatekeleza ujenzi wa mradi mkubwa wa maji katika kijiji cha Kidegembye wilayani Njombe ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu zaidi ya bilioni moja.
Ujenzi wa Mradi huo unagharamiwa na mfuko wa maji uliochini ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji , unajengwa na mkandalasi M/S STC Construction Limited utakamilika Novemba 2018 ambapo unatarajia kuhudumia watu zaidi ya 6,362 kwa kipindi cha miaka 20 ijayo .
Katika utekelezaji wa mradi huu wananchi wa kijiji cha Kidegembye wanachangia asilimia 2.5 ya gharama za mradi ambazo ni sawa na zaidi ya milioni 33 fedha ambazo zitatumika kuendeshea mradi baada ya kukabidhiwa.
Hadi sasa ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa lita laki moja na urefu wa mita sita uko katika hatua ya upigaji plasta, huku ujenzi wa mtego wa maji na nyumba ya pampu ukiwa katika hatua ya ukamilishaji.
Aidha, vifaa vyote kwa ajili ya mradi viko kwenye eneo la mradi ikiwemo mabomba yenye urefu wa mita 17 elfu huku uchimbaji wa mtaro na ulazaji wa bomba kuu ukikamilika na kazi inayoendelea ni upelekaji wa mabomba mitaani kwa wananchi.
Mbali na kunufaika kwa kupata huduma ya maji safi na salama, wananchi wa Kidegembye watapata manufaa ya fedha za kuanzia gharama za uendeshaji wa mradi huu baada ya kuingia mkataba na mkandalasi kwa kuchimba na kufukia mtaro ambapo fedha zitatazopatikana na kazi hiyo zitaingia kwenye mfuko wa Jumuiya ya watumia maji kama mchango wa wananchi kwa ajili ya usimamizi na uendeshaji wa mradi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa kijiji cha Kidegembye wameishukuru Serikali kwa kuwaletea mradi mkubwa wa maji ambao utasaidia kusukuma maendeleo kutokana na kuwa na uhakika wa maji safi na salama.
Halmashauri ya wilaya ya Njombe hadi sasa inajumla ya miradi 72 ya maji inayotumia teknolojia mbalimbali katika kutoa huduma ya maji safi na salama. Miradi inayotumia teknolojia ya maji mtiririko ipo 11, inayotumia mashine ya dizel ipo mitano, nishati ya umeme iko mitano.
Sambamba na hiyo miradi saba inatumia hydram inayosukumwa na nguvu ya maji, miradi mitatu inatumia nguvu ya maji kwa kutumia magurudumu ijulikanayo kama water wheel , huku miradi ya visima vifupi ipo 33 na virefu iko 8.
Kutokana na miradi hii watu 51,448 kati ya watu 85,747 sawa na asilimia 60 ya wananchi waliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe wanapata huduma ya maji.
Aidha, asilimia ya huduma ya maji imepanda kutoka 54.9 ya mwaka 2016/2017 hadi kufikia asilimia 60 mwaka 2018 kutokana na kukamilika kwa mradi wa maji katika kijiji cha Iwafi pamoja na uchimbaji wa kisima kirefu katika shule ya Msingi Kidegembye.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa