Baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Njombe limepitisha mpango na bajeti wenye kiasi cha zaidi ya bilioni 26 kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali katika mwaka wa fedha 2020/2021.
Katika bajeti hiyo kiasi cha bilioni 20.4 ni ruzuku ya mishahara, ruzuku ya miradi ya maendeleo ikiwa ni bilioni 2, matumizi mengineyo ikiwa ni milioni 716 na mapato ya ndani yakiwa zaidi ya bilioni 2.4 huku mchango wa jamii ikiwa ni zaidi ya milioni 500.
Akiwasilisha bajeti hiyo katika kikao maalum cha baraza la madiwani, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe , Ally Juma Ally alisema kuwa bajeti ya mwaka 2020/2021 imeongezeka kwa asilimia 24.77 ukilinganisha na bajeti iliyoidhinishwa na bunge ya mwaka 2019/2020 ambayo ilikuwa na kiasi cha zaidi ya bilioni 20.
“Mheshimiwa mwenyekiti ongezeko la bajeti limetokana na kuongezeka kwa makisio ya vyanzo vya mapato ikiwemo uwepo wa mradi wa tofali, mradi wa ukodishaji wa magari ya kubeba mawe , mchanga na tofali, mradi wa upimaji wa viwanja eneo la Mtwango pamoja na vyanzo vingine vya mapato” alieleza Ally.
Akielezea maeneo ambayo yamepewa kipaumbele katika Nyanja ya uchumi kwenye bajeti ya mwaka 2020/2021 alisema kuwa ni kuimarisha soko la mbao la Lunguya na kulifanya kuwa la kisasa, upimaji wa viwanja 150 katika Kijiji cha Lunguya kata ya Mtwango pamoja na kuimarisha mradi wa tofali uliopo Njombe Mjini.
Kuhusu miradi iliyopewa kipaumbele katika sekta ya afya Ally alieleza kuwa Halmashauri imepanga kukamilisha ujenzi wa hospitali ya Halmashauri inayojengwa katika kijiji cha Matembwe Kata ya Matembwe, ukamilishaji wa kituo cha afya katika Kata ya Kichiwa, ukamilishaji wa zahanati ya kijiji cha Lima pamoja na ujenzi wa vyoo bora katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Aidha, upande wa sekta ya elimu alitaja vipaumbele kuwa ni kuimarisha miundombinu ya kutolea elimu ikiwemo ujenzi wa hosteli katika shule za Ikuna na Manyunyu pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za Ikang’asi na Itova.
Upande wa miradi ya kimkakati, Ally alisema kuwa Halmashauri ya wilaya ya Njombe, imepanga kuendelea kukamilisha andiko la mradi wa ujenzi wa kituo cha biashara, kuandaa maandiko ya uboreshaji wa masoko ya mbao ya Nyombo na Mtwango pamoja na ujenzi wa hoteli ya kisasa katika eneo la makao makuu ya zamani yaliyopo Njombe Mjini.
Akichangia kuhusu bajeti hiyo mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe, Valentino Hongoli aliwapongeza wataalamu kwa kuandaa bajeti nzuri ambayo itakwenda kutatua changamoto za wananchi.
“Niwapongeze wataalam kwa kuandaa bajeti ambayo ni shirikishi yenye kuongeza mapato na kuboresha miundombinu katika Nyanja tofauti” alisema Hongoli
Halmashauri ya wilaya ya Njombe inajumla ya Kata 12, vijiji 45 pamoja na vitongoji 227.
Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Mtaa wa Idundilanga,Barabara ya Songea,Karibu na NMB.
Anuani ya Posta: S.L.P 547 Njombe
Namba ya Simu: +255 26 2782111
Simu Kiganjani:
Barua pepe: ded@njombedc.go.tz
Haki Miliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe. Haki zote zimehifadhiwa